Kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Kanuni ya Adhabu (The Penal Code), Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania kutokujua sheria hakuwezi kumwondolea hatia mtuhumiwa. Utaratibu huu hutumika katika mataifa yote pale ambapo shauri linasikilizwa mahakamani au katika vyombo vingine vyenye hadhi ya kimahakama (Quasi-Judicial bodies). Utaratibu huu hutumika katika masuala yote ya kisheria, ikujumuisha pia mashauri ya madai. Kwa hiyo, ni wajibu wa kila mtu katika jamii kujua sheria, angalau zile zinazozunguka maisha yake ya kila siku, ili inapotokea kwamba ameingia katika mgogoro basi ujuzi alionao umsaidie. Hakuna anayehurumiwa kwa kigezo cha kutokujua Sheria.
Kwa bahati mbaya, kutokana na uhaba wa wanasheria katika nchi yetu, na ukweli kwamba wengi kati ya wanasheria wachache waliopo wanafanyia shughuli zao mijini, sehemu kubwa ya Watanzania wamejikuta wakipata huduma hizi kwa gharama kubwa sana, na wakati mwingine kutozipata kabisa kwa namna inayostahili. Inambidi mwananchi mwenye shida ya huduma za kisheria awe na fedha za kugharimia safari, kujikimu njiani, malazi, tahadhari na fedha za kumlipa wakili. Hii ni gharama kubwa.
Kwa kuzingatia kwamba kujua sheria ni haki na wajibu wa kila mwanajamii, na kwa kufahamu kwamba upatikanaji wa elimu ya sheria ni tatizo kwa sehemu kubwa ya jamii ya Watanzania, hususan walio masikini na wale waishio vijijini, vijana wabunifu ambao wana elimu ya Utaalamu wa tehama na mifumo pamoja na Sheria waliamua kwa dhati kuanzisha mfumo wa huuwa upatikanaji wa huduma za kisheria kwa njia ya mtandao kwa watu wengi zaidi ikiwemo wale walio vijijini na sehemu za ndani za nchi ambazo ni ngumu sana kuweza kupata huduma hizi za kisheria lakini kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia tuu, ambayo itashusha gharama za huduma ya sheria kwa zaidi ya 80% (asilimia themanini) ukilinganisha na gharama za sasa.
Huduma hii itawezeshwa na matumizi yanayozidi kuongezeka ya teknolojia ya mawasiliano kwa mtandao (internet) na simu za mkononi.