Msimamizi wa mirathi ya marehemu ndiye mwakilishi wa marehemu kisheria na mali zote za marehemu ziko mikononi mwake na hivyo anapaswa kuwajibika kama ifuatavyo;
• Kukusanya mali zote za marehemu kwa uaminifu na uangalifu mkubwa.
• Kupeleka orodha ya mali ya marehemu au madeni aliyoweza kukusanya.
• Kupokea na kulipa madeni halali ya marehemu, ikiwa ni pamoja na kulipa gharama zitokanazo na usimamizi.
• Kugawanya mali iliyobaki kwa warithi halali wa marehemu.
• Kuifahamisha mahakama juu ya ugawaji wa mali za marehemu ulivyofanyika na kama umekamilika au muda zaidi uongezwe ili aweze kukamilisha ugawaji wa mali ya marehemu na kuiwezesha mahakama kufunga jalada la mirathi.
• Mtekelezaji au msimamizi wa mirathi anaweza kushitaki au kushitakiwa katika shauri lolote jipya au ambalo marehemu ama alianzisha au lilifunguliwa dhidi yake.
• Kadri atakavyoona inafaa, na kadri ilivyo kwa masilahi ya warithi, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi, anaweza kuuza mali inayohamishika kutoka katika mirathi ya marehemu.
• Mtekelezaji au msimamizi wa mirathi hawezi kutengeneza au kupata faida kutokana na usimamizi wake, isipokuwa kama wosia umesema hivyo.