Hatua zifuatazo zitapaswa kufuatwa katika mazingira ambapo marehemu hakuacha wosia: -Itokeapo kifo, taarifa ya kifo itolewe na kusajiliwa katika ofisi ya msajili wa vizazi na vifo ndani ya siku 30 toka kifo kitokee. Kumbuka kupewa hati ya kifo. -Kikao cha wana ukoo kifanyike ili kuchagua msimamizi wa mirathi na uamuzi huo uwekwe katika kumbukumbu kwa maandishi. -Msimamizi aliyeteuliwa na wana ukoo apeleke maombi ya kupata barua au hati ya usimamizi wa mirathi mahakamani akiambatanisha na cheti cha kifo na muhtsari wa kikao cha ukoo ambacho, pamoja na mambo mengine kilimteua muombaji kuwa msimamizi.wa mirathi -Mahakama itatoa taarifa kwa kubandika katika ubao wa matangazo mahakamani au gazetini juu ya maombi ya usimamizi wa mirathi na kutoa muda wa siku 90 kuruhusu mtu yeyote kutoa pingamizi. Kama hakuna pingamizi basi mahakama itatoa barua ya usimamizi wa mirathi kwa muombaji -Msimamizi wa mirathi husimamia ulipaji wa madeni ya marehemu na mgawanyo wa mali kwa warithi, na kisha kurejesha mahakamani nakala ya fomu inayoonyesha jinsi mgawo ulivyofanyika na kutiwa sahihi na kila mrithi.