Katika makabila yaliyo mengi Tanzania, ambayo hufuata mkondo wa kiume (patrilineal) mali za marehemu hugawanywa kwa kufuata upande wa ukoo wa kiumeni na warithi huwa ni watu wanaoangukia katika vyeo vya aina tatu ambavyo ni daraja la kwanza, daraja la pili na daraja la tatu.
• Daraja la kwanza: Cheo hiki hushikiliwa na mtoto wa kwanza wa kiume kutoka katika nyumba ya kwanza (kama ilikuwa ndoa ya wake wengi) au mtoto wa kiume aliyezaliwa kwanza kutoka nyumba yoyote iwapo marehemu hakuacha mtoto wa kiume katika nyumba ya kwanza.
• Daraja la pili: Cheo hiki hushikiliwa na watoto wa kiume waliosalia ambao hurithi sehemu kubwa kuliko watoto wa kike ambao huhesabika kama daraja la tatu.
• Daraja la tatu: Cheo hiki ndio cha mwisho na kinajumuisha watoto wa kike bila kujali tofauti ya umri na nafasi ya mama zao katika ndoa. Daraja hili hupata sehemu ndogo kuliko watoto wa kiume na kama watoto wa kiume hawapo basi watoto wa kike huongezewa Urithi.