Je, wanandoa wana haki zipi katika ndoa yao?
a) Wote wana haki ya kumiliki mali kama nyumba, shamba n.k. kwa majina yao binafsi
b) Wote wana haki ya kutoa idhini katika uuzaji au kwa pamoja kuweka dhamana mali yoyote ya familia
c) Wote wana haki ya kuendelea kuishi katika nyumba ya familia iwapo mume/mke amemtelekeza mwenzake
d) Mke ana haki ya kuendelea kupewa matunzo yake na ya watoto wakati wa ndoa hata inapotokea kwamba mume amemtelekeza au wameachana kwa amri ya mahakama. Na mume ana haki ya kupewa matunzo amepata ugonjwa ama ulemavu unaomfanya asiweze tena kujiingizia kipato
e) Wote wana haki ya kutokupigwa na/au kufanyiwa ukatili wa aina yoyote
f) Wote wana haki ya kupeana unyumba
g) Wote wana haki ya kutumia mali ya ndoa
h) Wote wana haki kuomba amri ya talaka.
Je ni Haki zipi za wanandoa zinazoambatana na amri ya talaka?
a)Mgawanyo wa mali za ndoa /familia
b) Matunzo ya mke
c)Hifadhi na matunzo ya watoto
d)Kizuizi cha kutobugudhiwa
e)Kuoa/Kuolewa tena
f) Fidia ya uzinzi
g)Gharama za kuendesha Shauri la Talaka
Sababu ipi mahakama inatumia ili kutoa talaka?
a)Ugoni
b)Ukatili
c)Ulawiti
d)Kifungo cha maisha au cha miaka mitano
e)Kubadili dini
f)Kutengana kwa hiari au kwa amri ya mahakama
g)Kipigo
Je haki za mwanamke katika ndoa ni zipi?
a)Usawa
b)Matunzo
c)Kumiliki Mali
d)Kuishi katika nyumba ya ndoa
e)Kukopa
f)Kupata haki ya jasho lake
Je, ni masharti gani ya kuzingatia kabla ya kubadili aina ya ndoa?
Kabla ndoa haijabadilishwa ni lazima kwanza wanandoa wakubaliane na watoe tamko kwa maandishi mbele ya jaji au hakimu juu ya uamuzi wao huo na wote watie saini zao.
Je sheria inatambua aina ngapi za ndoa?
Kuna aina mbili tu za ndoa zinazotambulika, nazo ni
a) ndoa ya mke mmoja, na
b) ndoa ya wake wengi: Aina hii ya ndoa inaruhusu mwanaume kuwa na mke zaidi ya mmoja. Kwa mfano, ndoa za kimila na za dini ya kiislam
Kuna aina ngapi za ufungishaji wa ndoa?
Kuna aina tatu za ufungishaji ndoa, ambazo ni:
a) Ufungishaji Ndoa Kidini: Ndoa zinazofungishwa kidini hufuata taratibu za dini au madhehebu husika ambayo wanandoa ni waumini wa dini hiyo au madhehebu hayo.
b) Ufungishaji Ndoa Kiserikali: Sheria ya ndoa pia inaruhusu wanandoa kufunga ndoa kwa kufuata taratibu za kiserikali. Mara nyingi ndoa za kiserikali zinakuwa zikifungwa kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya na zimekuwa zikifahamika maarufu kama ndoa za bomani.
c) Ufungishaji Ndoa Kimila :Hizi ni ndoa zinazofungwa kwa kufuata taratibu za kabila husika ambalo wanandoa wanatoka
Je kuna faida zipi za kusajili ndoa?
Kusajili ndoa kuna faida zifuatazo;
a) Usajili wa ndoa na cheti cha ndoa unarahisisha taratibu na mashauri yanayohusu mirathi kwa kujua aina ya ndoa na yupi ni mke/mme halali,hivyo kusaidia kulinda haki ya mjane au mgane.
b) Umiliki wa mali: kusajili ndoa yako kunasaidia katika kutambulisha wanandoa halali na pia inasaidia katika kujua nani ana haki ya kumiliki mali za ndoa
c) Ushahidi: Usajili pia unasaidia katika kuweka ushahidi kwamba wahusika ni wanandoa. Katika mashauri ya talaka cheti kitahitajika mahakamani katika kuthibitisha hadhi ya wadaawa.
Je kuna aina ngapi za kutengana ?
Kutengana kupo kwa aina mbili;
i. Kwa hiari ya wanandoa wenyewe.
ii. Kwa amri ya mahakama.
Nini maana ya kutengana kwa wana ndoa?
Kutengana ni ile hali ya wanandoa kuacha kuishi pamoja, yaani kuacha kuishi chini ya dari moja.
Je ni vigezo vipi ili mahakama iweze kusikiliza shauri la kuomba talaka?
Kwa mujibu wa kifungu cha 100 mahakama haiwezi kusikiliza shauri la talaka kama ndoa haijadumu kwa miaka miwili. Ili shauri la talaka lipokelewe kabla ya miaka miwili ya ndoa kupita ni lazima mahakama itoe idhini. Idhini hiyo hutolewa pale tu ambapo
mwanandoa mmoja anapata mateso yasiyo
kuwa ya kawaida.
Je kutengana kwa wana ndoa kunaondoa wajibu kwa mwanandoa?
Kwa mujibu wa kifungu cha 111 Amri ya kutengana inawafanya wanandoa wasikae tu pamoja lakini haiondoi wajibu na majukumu aliyo nayo mwanandoa kuhusiana na matunzo.
Ni hatua zipi za kuchukua kabla ya kufunga ndoa?
Lazima taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe siku 21 kabla ya ndoa kufungwa, kama kutakuwa na mwenye pingamizi sharti litolewe itoe kabla ya ndoa kufungwa. Taarifa hiyo inapaswa kutaja:
-Majina ya wale wanaotarajia kufunga ndoa, umri, majina ya wazazi wao na mahali wanapoishi yatajwe.
Tamko kwamba wanaotarajia kufunga ndoa hawana uhusiano unaokatazwa kisheria kufunga ndoa
Mahakama zipi zenye mamlaka ya kusikiliza madai ya talaka
Mahakama zenye mamlaka kusikiliza mashauri ya ndoa ni
a)Mahakama ya Mwanzo
b)Mahakama ya Wilaya
c)Mahakama ya Hakimu Mkazi na
d)Mahakama Kuu
Mahakama hizi zote zina mamlaka sawa , yaani mtu anaweza kufungua shauri lake katika mojawapo ya mahakama hizo.
Je ni vigezo gani vya kuzingatia kabla ya kufunga ndoa?
Mambo ambayo ni ya msingi ili kufanya muunganiko wa mwanaume na mwanamke uweze kutambuliwa kama Ndoa ni pamoja na haya yafuatayo:
a) Hiari : lazima muunganiko utokane na chaguo binafsi la wahusika; bila Udanganyifu, laghai au kurubuniwa kwa aina yoyote
b) Kusudio la kudumu: muunganiko wa wanandoa sharti uwe umekusudiwa kuwa wa kudumu, isipokuwa kama litatokea jambo ambalo liko nje ya uwezo wa wanandoa kuzuia kuvunjika kwa muunganiko huo, kama vile kifo cha mmoja wao, talaka, nk.
c) Jinsi Tofauti: Ndoa sharti iwe kati ya mtu-mme na mtu-mke; watu wenye maumbile tofauti ya via vya uzazi
d) Isihusishe Maharimu: Sheria inazuia ndoa kati yadada na kaka, baba na binti yake, mama na mwanawe, babu au bibi na mjukuu wake, shangazi au mjomba na mpwawe, au baba ama mama mlezi na mtoto aliyemuasili.
e) Umri: Kigezo cha umri kimetajwa katika muktadha tofautitofauti, lakini kwa ujumla, wanandoa wanapaswa kuwa na umri wa miaka 18 au zaidi.
f) Uwepo wa Ndoa nyingine: Kama mwanamne ana ndoa nyinigne isiyomruhusu kuongeza mke, au kama mwanamke ana mme mwingine basi ndoa hiyo haiwezi kufungwa.
g) Kusiwe na Pingamizi: Kabla ya ndoa kufungwa ni lazima tangazo litolewe juu ya kusudio la kufunga ndoa, na ndoa hiyo haitafungwa iwapo kutakuwa na pingamizi halali kutoka kwa mtu mwenye haki ya kufanya hivyo.
h) Mfungishaji ndoa awe na mamlaka ya kufanya hivyo: Mfungishaji wa ndoa ni lazima awe na leseni au kibali cha kufungisha ndoa kutoka kwa msajili mkuu wa ndoa.
i) Kuwe na mashahidi: Ni lazima wakati wa kufunga ndoa kuwe na mashahidi wasiopungua wawili ambao ni lazima wawe na umri si chini ya miaka 18 na wawe na akili timamu na kuelewa lugha inayotumika katika shughuli hiyo. Pia ni lazima wawepo kwa pamoja kwenye tukio la kufunga ndoa.
j) Sharti wafunga ndoa wote wawili wawepo: Wanandoa wote wawili sharti wawepo kwa pamoja wakati wa tukio la kufunga ndoa
Je ni lazima kusajili ndoa?
Ndiyo. Kila ndoa iliyofungwa; iwe yakidini, kiserikali au kimila inatakiwa isajiliwe kwenye daftari la Msajili Mkuu wa Ndoa ndani ya siku 30 baada ya kufungwa.
Je mwanamke na mwanaume walioishi pamoja kwa kipindi fulani bila kufunga ndoa wanaweza kuhesabika kuwa wanandoa?
Ndiyo. Pale ambapo mwanamke na mwanamme, wenye sifa za kufunga ndoa, wameishi pamoja kwa miaka isiyopungua miiwili kwa namna ambayo inawatambulisha kama mke na mme watachukuliwa kama wanandoa hadi pale itakapothibitika vinginevyo.
Je sheria inaruhusu kubadili aina ya ndoa?
Ndiyo. Wanandoa wanaruhusiwa kubadili aina ya ndoa yao; kama ilikuwa ya mke mmoja kuwa ya wake wengi au kama ilikuwa imekusudiwa kuwa ya wake wengi, kuwa ya mke mmoja.
Je ndoa batili ni ipi?
Ndoa batili ni ile iliyofungwa kinyume na matakwa ya kisheria
Je nini maana ya Ndoa batilifu?
Ndoa batilifu ni ndoa halali na itaendelea kuwa hivyo hadi hapo mahakama itakapoitengua kwa kuombwa na mwanandoa mmojawapo.
Je ndoa ni nini kwa mujibu wa sheria za Tanzania?
Ndoa ni muunganiko wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao yote.
Je mamlaka za ufungishaji wa ndoa ni zipi?
Sheria imebainisha na kutoa nguvu kwa mamlaka zifuatazo kuwa na uwezo wa kufungisha ndoa:
a) Msajili mkuu au msajili msaidizi katika ofisi za wilaya/ Manispaa
b) Viongozi wa dini katika makanisa na Misikiti
c) Viongozi wa mila katika kabila husika
Je nini maana ya dhana ya ndoa?
Sheria ya ndoa katika kifungu cha 160 inaeleza juu ya mahusiano haya kwamba endapo mwanamke akiishi na mwanaume kwa miaka miwili au zaidi mfululizo na jamii inayowazunguka ikawatambua na kuwapa hadhi ya mume na mke, basi mahusiano hayo yaweza kupata dhana ya kuchukuliwa kama wanandoa.
Nini maana ya talaka na mamlaka yenye uwezo wa kutoa talaka?
Talaka ni amri ya mahakama ya kuvunja ndoa. Chombo pekee chenye uwezo wa kuvunja ndoa ni mahakama tu. Ni lazima talaka itolewe na mahakama ili haki ya kila mwanandoa itamkwe bayana.
Mambo gani yanaweza kupelekea ndoa kuwa batilifu?
Yafuatayo yanaweza kubatilisha ndoa:
a) Kutokuwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa
b) Mmoja wa wanandoa kudhihirika kuwa na kichaa au kifafa.
c) Mmoja wa wanandoa kudhihirika kuwa alikuwa ana ugonjwa wa zinaa
d) Mke kudhihirika kuwa alikuwa na mimba ya mwanaume mwingine.
e) Mwanandoa mmoja kukataa kwa makusudi kufanya tendo la
ndoa baada ya ndoa kufungwa