Je, ni taratibu zipi huchukuliwa pale kunapotokea pingamizi katika maombi ya usimamizi wa mirathi?
- Baada ya pingamizi kuwekwa dhidi ya maombi ya usimamizi wa mirathi, muombaji anapaswa kuiomba mahakama imuite aliyeweka pingamizi hilo ili aiambie mahakama kama anakubaliana na maombi ya usimamizi wa mirathi au hakubaliani nayo na atoe sababu za kutokukubaliana na maombi hayo.
-Maombi ya usimamizi wa mirathi hubadilika na kuchukua mfumo wa shauri la dau. Aliyeweka pingamizi hugeuka kuwa mdai na muombaji wa usimamizi wa mirathi hugeuka kuwa mshtakiwa.
-Muweka pingamizi anaposhindwa kufika mahakamani au anapokubaliana na maombi ya usimamizi wa mirathi pingamizi lake litahesabika kama limefutwa na mahakama itaendelea na shauri la maombi ya usimamizi wa mirathi na muweka pingamizi hataruhusiwa kuleta pingamizi tena.
Je, ni sababu zipi zinazoweza kufanya maombi ya usimamizi wa mirathi kubadilika na kuwa shauri la dau mahakamani?
- Madai ya wosia uliogushiwa
- Madai ya kwamba wosia uliandaliwa wakati muusia hana akili timamu au kwa kulazimishwa.
- Madai ya wosia kutokidhi sifa zinazohitajika.
- Matumizi mabovu ya mali za marehemu na msimamizi wa mirathi.
Taratibu gani hufuatwa baada ya pingamizi kwa maombi ya mirathi kuwekwa?
-Baada ya pingamizi kuwasilishwa mahakamani, maombi ya mirathi huchukua mfumo wa shauri la kawaida la dau na mwombaji wa mirathi hupewa muda wa kujibu malalamiko ya mweka pingamizi.
-Mahakama husikiliza pingamizi hilo na inaporidhika na sababu zilizotolewa katika pingamizi inaweza kubatilisha uthibitishwaji wa mtekeleza mirathi au kukataa uteuzi wa mwombaji wa usimamizi wa mirathi.
Je, marehemu anapofariki bila kuacha wosia ni mambo gani ya muhimu huambatanishwa na maombi ya kuwa msimamizi wa mirathi?
-Nakala ya cheti cha kifo cha marehemu
-Nakala ya kikao cha wanandugu cha kumchagua msimamizi wa mirathi
-Tamko la mwombaji kwamba atasimamia mirathi kwa uaminifu
-Kiapo cha wanandugu kwamba wamemteua mwombaji kuwa msimamizi wa mirathi
-Kiapo cha mashahidi wakimdhamini mwombaji na kwamba wako tayari kutoa
fidia endapo mwombaji atashindwa kusimamia vizuri ugawaji wa mali hizo.
Je, ni taarifa au nakala zipi za muhimu zinazohitajika katika shauri la mirathi?
-Nakala ya muhtasari wa kumbukumbu wa kikao cha ukoo.
-Nakala ya wosia, iwapo marehemu aliacha wosia.
-Majina ya warithi halali wa mali za marehemu
-Cheti cha kifo
-Cheti cha ndoa, iwapo marehemu aliacha mke/mume
-Vyeti vya kuzaliwa vya watoto
-Taarifa muhimu za marehemu: majina, tarehe ya kufariki, jina la mwombaji, orodha ya mali alizoacha marehemu
-Nakala au taarifa zozote zitakazo hitajika mahakamani
Je, ni watu gani wanaweza kuwa wasimamizi wa mirathi?
-Ndugu wa marehemu na wale wenye maslahi na mirathi ya marehemu, kwa mfano wale ambao wanatarajia kupata sehemu ya mirathi ya marehemu.
-Mtu au watu wanaomdai marehemu, mtu huyu hufungua mirathi pale ambapo ndugu wa marehemu wameshindwa au hawataki kufungua mirathi.
-Kabidhi wasii mkuu.
-Muwakilishi wa kisheria au mtu aliyetajwa kama msimamizi wa mirathi kwenye wosia.
-Mtu yeyote ambaye mahakama kwa kuangalia vigezo mbalimbali vikiwamo undugu,maslahi ya muhusika katika mirathi hiyo, usalama wa mali za mirathi pamoja na uwezekano wa kusimamia vizuri, anaweza kuteuliwa na mahakama.
Je, mali za marehemu hugawanywa kwa mfumo upi chini ya sheria ya kiislamu?
-Wajane au mjane hurithi kama marehemu ameacha watoto
-Wajane au mjane hurithi robo kama marehemu hakuacha watoto
-Wazazi hupewa salio baada ya kuondoa fungu la mjane au wajane
-Mali inayobaki hugawanywa katika mafungu matatu. Watoto wa kiume hupata mafungu mawili na watoto wa kike hupata fungu moja
-Mgane hupewa robo ya mali ya marehemu mke wake kama kuna watoto au nusu kama hakuna watoto.
Ni nini faida za kuandaa wosia?
-Wosia humpa muusia fursa ya kufanya mgao wa mali yake kwa kadri anavyotaka kabla ya kufariki.
-Muusia anapata fursa ya kuamua ni nani msimamizi wa mirathi yake.
-Wosia huepusha ugomvi wa wana familia.
-Wosia ni chombo cha kuhakikisha kwamba urithi unakwenda kwa watu ambao marehemu aliwaridhia.
Je, msimamizi wa mirathi akiwa chini ya miaka 18 au mlemavu ataruhusiwa kugawa mali za marehemu?
Endapo amechaguliwa mtoto wa chini ya miaka 18 au mtu mwenye ulemavu unaoathiri uwezo wake wa kusimamia majukumu yake kuwa msimamizi wa mirathi, inashauriwa kuwa na msimamizi wa ziada ili kusaidia kuhakikisha kuwa usimamizi wa mali za marehemu unafanyika kwa namna inayokidhi matarajio na matakwa ya kisheria.
Je, warithi wana haki gani dhidi ya msimamizi wa mirathi?
Endapo msimamizi wa mirathi amesimamia au ametumia mirathi ya marehemu vibaya, warithi halali wa marehemu, pamoja na mambo mengine, wanaweza kufanya yafuatayo;
-Wanaweza kuiomba mahakama kumfutia utekelezaji au usimamizi wa mirathi na hivyo kulazimika kurudisha mahakamani hati zote zilizotolewa na mahakama kuthibitisha utekelezaji au usimamizi wake wa mirathi, ili mahakama iweze kumchagua mtu mwingine.
-Kama amekataa kurudisha mahakamani hati zote zilizotolewa na mahakama kuthibitisha utekelezaji au usimamizi wake wa mirathi, warithi wanaweza kumshitaki na akikutwa na hatia anaweza kutozwa faini au kifungo kisichozidi miezi mitatu au vyote faini na kifungo.
-Kama mtekelezaji huyo na/au msimamizi wa mirathi amesimamia vibaya au ameharibu mali ya marehemu, warithi au mtu yeyote mwenye maslahi na usimamizi huo, anaweza kumfikisha mahakamani akimtaka alipe fidia kwa uharibifu au hasara aliyosababisha.
Ni sheria gani zinazosimamia masuala ya Mirathi Tanzania?
Hadhi na Imani ya marehemu wakati wa kifo chake ndiyo inayoamua Sheria gani itumike katika kushughulikia mirathi yake. Kwa ujumla, mojawapo ya, Sheria zifuatazo hutumika;
- Sheria ya serikali
- Sheria ya Kimila
- Sheria ya dini ya kiislamu.kuhusu mirathi
Je, ni lazima msimamizi wa mirathi awe ndugu wa marehemu?
Hapana. Msimamizi wa mirathi siyo lazima awe ndugu wa marehemu. Kwa hakika, Anaweza hata kuwa taasisi au ofisi fulani kama vile benki, ilimradi taasisi hiyo iweze kushughulikia mali za marehemu kwa kuzingatia haki na sheria.
Ikiwa marehemu aliacha wosia, ni taratibu zipi hufuatwa katika kufungua mirathi?
Hatua zifuatazo zitapaswa kufuatwa katika mazingira ambapo marehemu ameacha wosia:
-Taarifa ya kifo ikaandikishwe kwa Msajili wa vizazi na vifo katika muda wa siku 30.
-Kama wosia umemtaja mtu atakayekuwa msimamizi wa mirathi, msimamizi huyo afungue mirathi mahakamani akiwa na wosia ulioachwa, pamoja na cheti cha kifo.
-Ikiwa hakuna mtu aliyetajwa kuwa msimamizi wa mirathi, utaratibu wa wanandugu kukaa kikao ufanyike kumteua mtu atakayekuwa msimamizi wa mirathi.
-Mahakama hutoa tangazo la mirathi kwa muda wa siku 90 na kama hakuna pingamizi lolote, msimamizi hukabidhiwa barua ya kuhalalisha kugawa urithi na kulipa madeni.
-Baada ya ugawaji wa mali, msimamizi hupaswa kupeleka taarifa za ugawaji wa mali mahakamani na mahakama hufunga jalada baada ya kujiridhisha kwamba msimaizi wa mirathi ametekeleza majukumu yake kwa uaminifu na kwa mujibu wa Sheria.
Ikiwa marehemu hakuacha wosia, ni taratibu zipi hufuatwa katika kufungua mirathi?
Hatua zifuatazo zitapaswa kufuatwa katika mazingira ambapo marehemu hakuacha wosia:
-Itokeapo kifo, taarifa ya kifo itolewe na kusajiliwa katika ofisi ya msajili wa vizazi na vifo ndani ya siku 30 toka kifo kitokee. Kumbuka kupewa hati ya kifo.
-Kikao cha wana ukoo kifanyike ili kuchagua msimamizi wa mirathi na uamuzi huo uwekwe katika kumbukumbu kwa maandishi.
-Msimamizi aliyeteuliwa na wana ukoo apeleke maombi ya kupata barua au hati ya usimamizi wa mirathi mahakamani akiambatanisha na cheti cha kifo na muhtsari wa kikao cha ukoo ambacho, pamoja na mambo mengine kilimteua muombaji kuwa msimamizi.wa mirathi
-Mahakama itatoa taarifa kwa kubandika katika ubao wa matangazo mahakamani au gazetini juu ya maombi ya usimamizi wa mirathi na kutoa muda wa siku 90 kuruhusu mtu yeyote kutoa pingamizi. Kama hakuna pingamizi basi mahakama itatoa barua ya usimamizi wa mirathi kwa muombaji
-Msimamizi wa mirathi husimamia ulipaji wa madeni ya marehemu na mgawanyo wa mali kwa warithi, na kisha kurejesha mahakamani nakala ya fomu inayoonyesha jinsi mgawo ulivyofanyika na kutiwa sahihi na kila mrithi.
Ikiwa marehemu amefariki na kuacha wosia, mali zake zitagawanywa kwa kutumia sheria ipi?
Ikiwa marehemu ameacha wosia, mali zake zitagawanywa kwa mujibu wa wosia ulioachwa.
Mali za marehemu hupelekwa wapi ikibainika kuwa hakuacha ndugu yeyote au mtoto?
Ikiwa marehemu amefariki bila kuacha ndugu yeyote wala mtoto, mali zake zitasimamiwa na kabidhi mkuu wa serikali.
Je, ni taratibu zipi huchukuliwa pale ambapo msimamizi wa mirathi aliyechaguliwa na familia au aliyeteuliwa kwenye wosia atakataa kutimiza wajibu huo?
Inapotokea msimamizi wa mirathi amekataa kutimiza wajibu huo, mmoja kati ya warithi au mtu yeyote mwenye maslahi kwenye mirathi ya marehemu anaweza kuomba mahakama imuite msimamizi huyo kujibu sababu za kutokutimiza majukumu hayo au imvue msimamizi huyo majukumu hayo na kumpa mtu mwingine aliye tayari kuyatekeleza majukumu hayo.
Je, ni lazima mirathi ifunguliwe mahakamani?
Kama marehemu ameacha mali ambayo inatakiwa kurithiwa ni lazima shauri la mirathi lifunguliwe mahakamani ili kupata barua ya usimamizi wa mirathi. Si halali kugawanya au kuuza mali ya marehemu bila kufuata utaratibu huu.
Je, mgawanyo wa mali kwa kutumia sheria ya kimila huchukua mfumo upi?
Katika makabila yaliyo mengi Tanzania, ambayo hufuata mkondo wa kiume (patrilineal) mali za marehemu hugawanywa kwa kufuata upande wa ukoo wa kiumeni na warithi huwa ni watu wanaoangukia katika vyeo vya aina tatu ambavyo ni daraja la kwanza, daraja la pili na daraja la tatu.
-Daraja la kwanza: Cheo hiki hushikiliwa na mtoto wa kwanza wa kiume kutoka katika nyumba ya kwanza (kama ilikuwa ndoa ya wake wengi) au mtoto wa kiume aliyezaliwa kwanza kutoka nyumba yoyote iwapo marehemu hakuacha mtoto wa kiume katika nyumba ya kwanza.
-Daraja la pili: Cheo hiki hushikiliwa na watoto wa kiume waliosalia ambao hurithi sehemu kubwa kuliko watoto wa kike ambao huhesabika kama daraja la tatu.
-Daraja la tatu: Cheo hiki ndio cha mwisho na kinajumuisha watoto wa kike bila kujali tofauti ya umri na nafasi ya mama zao katika ndoa. Daraja hili hupata sehemu ndogo kuliko watoto wa kiume na kama watoto wa kiume hawapo basi watoto wa kike huongezewa Urithi.
Kuna aina ngapi za wosia?
Kuna aina mbili za wosia ambazo ni;
-Wosia wa maandishi
-Wosia wa mdomo.
Je, kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, mtoto wa nje ya ndoa ana haki ya kurithi?
Kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, watoto waliozaliwa nje ya ndoa hawana haki ya kurithi chochote kutoka katika mirathi ya baba yao.
Nini lengo kuu la uwepo wa sheria za Mirathi?
Lengo kuu la uwepo wa sheria za mirathi ni kuweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba mali na madeni ya marehemu vinasimamiwa kwa namna ambayo inazuia uwezekano wa kuhatarisha amani au kusababisha hasara kwa warithi wa marehemu na/au wadeni wake.
Nini wajibu wa mahakama katika kuchagua msimamizi wa mirathi?
Mahakama inao wajibu wa kuchunguza kwa makini na kujiridhisha kwamba mtu anayeomba kuthibitishwa au kuteuliwa kuwa mtekelezaji au msimamizi wa mirathi, anayo maslahi katika mirathi hiyo na ataweza kufanya kazi hiyo kwa makini na uaminifu mkubwa kulingana na matakwa ya marehemu (kama yanaweza kubainika) katika kusimamia mali hizo.
Je, ni wakati gani mahakama inaweza kubatilisha uthibitishwaji wa msimamizi wa mirathi?
Mahakama yaweza kubatilisha uthibitishwaji wa mtekelezaji mirathi endapo itabaini yafuatayo;
-Kwamba mwenendo wa kupata utekelezaji au usimamizi wa mirathi ulikuwa na dosari za msingi.
-Kwamba utekelezaji au usimamizi wa mirathi ulipatikana kwa udanganyifu baada ya kutoa mapendekezo ya uwongo au baada ya kuificha mahakama habari muhimu na za msingi katika mirathi hiyo.
-Kwamba utekelezaji au usimamizi wa mirathi ulipatikana kwa njia ya malalamiko ya uwongo juu ya jambo la muhimu la kisheria ili kuthibitisha kupatikana kwa utekelezaji au usimamizi wa mirathi, ingawa malalamiko hayo yalifanywa kwa kutojua au bila nia mbaya.
-Kwamba utekelezaji au usimamizi wa mirathi umekuwa hauna maana na haitekelezeki.
-Kwamba mtu aliyepewa utekelezaji au usimamizi wa mirathi, kwa makusudi ameamua kutopeleka orodha ya mali za marehemu au amepeleka mahakamani orodha au taarifa ya uwongo ya mgawanyo wa mali za marehemu.
Je, mali ya marehemu inaweza kuuzwa kabla ya maombi ya usimamizi wa mirathi kukubalika mahakamani?
Marehemu anapoacha mali inayoweza kuharibika au kuteketea kirahisi mfano mazao, msimamizi wa mirathi anaweza kuomba kibali cha mahakama cha kusimamia mirathi kwa muda ikiwemo kuuza mali hizo ikiwa tu itaonekana uuzaji huo ni wa manufaa kwa warithi.
Je, mgawanyo wa mali kwa kutumia sheria ya kiislamu huzingatia mambo yapi?
Mgawanyo wa mali kwa sheria ya kiislamu huzingatia mambo yafuatayo;
-Sharti ithibitike kwamba mwenye mali ameshafariki (maut-al-muwarith)
-Kuwepo na warithi halali wa marehemu, yaani watoto wa marehemu na ndugu wengine na wote wawe warithi hakika wanaotambulika kisheria wakati wa mauti ya marehemu. (hayat-al-warith)
-Marehemu awe ameacha mali
-Urithi utokane na mali halisi na halali za marehemu.
Je, mgawanyo wa mali kwa kutumia sheria ya serikali huchukua mfumo upi?
Mgawanyo wa mali kwa sheria ya serikali huwa kama ifuatavyo;
-Kama marehemu ameacha mjane na watoto, mjane atapata ya mali zote za marehemu na watoto watapata ya mali zote za marehemu.
-Kama marehemu hakuacha watoto, mjane atapata nusu ya mali zote za marehemu na nusu nyingine hugawanywa sawasawa kati ya wazazi, kaka na dada za marehemu.
Je, muombaji wa usimamizi wa mirathi aliyenyimwa kibali na mahakama au msimamizi aliyevuliwa mamlaka hayo ana haki gani dhidi ya maamuzi hayo?
Msimamizi wa mirathi aliyevuliwa mamlaka hayo au muombaji aliyekataliwa maombi hayo kwa njia ya pingamizi anaweza kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya mahakama.
Je, ni lazima msimamizi wa mirathi awe mtu mmoja?
Msimamizi wa mirathi siyo lazima awe mtu mmoja. Wanaweza kuchaguliwa watu hata wawili au zaidi kushirikiana katika majukumu ya usimamizi wa mirathi.
Je, ni taratibu gani huchukuliwa pale ambapo marehemu sio mtanzania ila ana mali zake Tanzania na amezirithisha katika wosia wake?
Msimamizi wa mirathi wa marehemu huyo anawajibika kuomba mahakama ya Tanzania kumtambua kama msimamizi wa mirathi hio. Maombi hayo huambatanishwa na kibali cha usimamizi wa mirathi kilichotolewa na mahakama ya nchi ambayo marehemu alikua raia wake. Taratibu hii hukubalika na kufuatwa na nchi zilizo katika jumuiya ya madola ikiwemo Tanzania.
Nini wajibu wa msimamizi wa mirathi?
Msimamizi wa mirathi ya marehemu ndiye mwakilishi wa marehemu kisheria na mali zote za marehemu ziko mikononi mwake na hivyo anapaswa kuwajibika kama ifuatavyo;
-Kukusanya mali zote za marehemu kwa uaminifu na uangalifu mkubwa.
-Kupeleka orodha ya mali ya marehemu au madeni aliyoweza kukusanya.
-Kupokea na kulipa madeni halali ya marehemu, ikiwa ni pamoja na kulipa gharama zitokanazo na usimamizi.
-Kugawanya mali iliyobaki kwa warithi halali wa marehemu.
-Kuifahamisha mahakama juu ya ugawaji wa mali za marehemu ulivyofanyika na kama umekamilika au muda zaidi uongezwe ili aweze kukamilisha ugawaji wa mali ya marehemu na kuiwezesha mahakama kufunga jalada la mirathi.
-Mtekelezaji au msimamizi wa mirathi anaweza kushitaki au kushitakiwa katika shauri lolote jipya au ambalo marehemu ama alianzisha au lilifunguliwa dhidi yake.
-Kadri atakavyoona inafaa, na kadri ilivyo kwa masilahi ya warithi, mtekelezaji au msimamizi wa mirathi, anaweza kuuza mali inayohamishika kutoka katika mirathi ya marehemu.
-Mtekelezaji au msimamizi wa mirathi hawezi kutengeneza au kupata faida kutokana na usimamizi wake, isipokuwa kama wosia umesema hivyo.
Je, mtoto wa nje ya ndoa ana haki ya kurithi?
Mtoto wa nje ya ndoa hana haki ya kurithi, isipokuwa tu kama ametajwa na kugawiwa fungu katika wosia wa marehemu.
Je, ni mahakama ipi inayomruhusu mtu kufungua mirathi?
Mtu anaweza kufungua mirathi katika mahakama ya mwanzo, mahakama ya wilaya au hata ya hakimu mkazi kwa kuzingatia mahali marehemu alipokua anaishi isipokua mirathi inayofuata sheria za mila au dini ya kiislamu hufunguliwa katika mahakama ya mwanzo.
Je, muusia anaweza kumnyima mrithi halali sehemu ya urithi wake?
Muusia anaweza kumnyima mrithi sehemu ya urithi wake ikiwa mrithi;
-Amezini na mke wa muusia.
-Amejaribu kumuua, amemshambulia au amemdhuru vibaya muusia au mama mzazi wa mrithi.
-Bila sababu ya haki, hakumtunza muusia kutokana na njaa au ugonjwa.
-Ameharibu mali ya muusia. Uharibifu huo utahesabika katika kukadiria kiwango cha urithi atakachostahili kupata.
Je, ni lazima muusia kurithisha mali zake zote?
Muusia anaweza kuusia mali yake bila kutaja kila kitu alichonacho wakati wa kufa kwake na baada ya mali hio kugawanywa kwa mujibu wa wosia ulioachwa, sehemu iliyobaki itagawanywa kulingana na masharti ya urithi usio na wosia.
Je, kuna kikomo cha muda wa kufungua mirathi mahakamani?
Sheria inatoa kikomo cha muda wa miaka mitatu tangu marehemu afariki kama muda ambao mirathi inaweza kufunguliwa mahakamani. Muda huo unaweza kuongezwa pale itakapobainika kuwa kuna sababu za msingi zilizosababisha mirathi kuchelewa kufunguliwa mahakamani.
Je, mwanamke anaweza kurithi ardhi chini ya sheria ya kimila?
Sheria ya Ardhi ya Vijijini (Namba 5 ya mwaka 1999) imesahihisha utaratibu wa umiliki ardhi wa kimila (urithi wa ardhi) kwa kuondoa ubaguzi wa aina yoyote kwenye umiliki wa ardhi na kuweka usawa kwa wanawake na wanaume. Kwa msingi huu, cheo cha tatu cha urithi kwenye sheria za kimila kinakuwa batili pale urithi wa mali ya marehemu unapohusisha suala la ardhi.
Je, mwanamke anaweza kurithi ardhi chini ya sheria ya mila?
Sheria ya ardhi ya vijijini namba 5 ya mwaka 1999 imesahihisha utaratibu wa umiliki ardhi wa kimila (urithi wa ardhi) kwa kuondoa ubaguzi wa aina yoyote kwenye umiliki wa ardhi na kuweka usawa kwa wanawake na wanaume. Kwa misingi hii, cheo cha tatu cha urithi kwenye sheria za kimila kinakua batili pale urithi wa mali ya marehemu unapogusia suala la ardhi.
Je, sheria ya kimila inatumika katika mazingira gani?
Sheria ya kimila hutumika kwa mtu ambaye wakati wa maisha yake aliishi kwa mujibu wa mila na desturi za kabila fulani, na hakuandika wosia kabla ya kifo chake.
Je, mjane ana nafasi gani katika sheria ya mila?
Sheria ya kimila katika tangazo la serikali namba 436 la mwaka 1963 haimruhusu mjane kurithi mali za marehemu mume wake. Mjane mwenye watoto inabidi aishi kwa kutegemea watoto wake. Mjane ambaye hana watoto atabaki katika nyumba ya marehemu na kupewa asilimia 20 ya nusu ya mali ya marehemu na kuitumia wakati wa uhai wake, akifariki au akiolewa na mtu mwingine nje ya ukoo wa marehemu mali hiyo na nyumba aliyokua anakaa hugawiwa kwa warithi halali wa marehemu mume wake.
Je, kwa mujibu wa sheria ya mila, mtoto wa nje ya ndoa ana haki ya kurithi?
Sheria ya mila inatamka kua, watoto waliozaliwa nje ya ndoa hawaruhusiwi kurithi isipokua tu pale marehemu anapoacha wosia unaowapa haki ya kurithi au, Ikiwa walihalalishwa na marehemu kabla ya kufa.
Je, ni mtiririko upi unaotumika katika kulipa madeni ya marehemu?
Sheria ya urithi na usimamizi wa mirathi imebainisha jinsi ambavyo madeni ya marehemu yanatakiwa kulipwa kwa kutoa kipaumbele kama ifuatavyo Kwanza- Gharama za mazishi na matibabu.Pili- Gharama za ufunguzi na usimamizi wa shauri la mirathi zikiwemo gharama za kuendesha shauri hilo.Tatu- Malipo kwa huduma zilizotolewa kwa marehemu na mfanyakazi, kibarua au mtumishi wa nyumbani.Nne- Malipo kwa madeni mengine yaliyoachwa na marehemu.
Je, nini maana ya Urithi?
Urithi ni mali na madeni anayoacha mtu baada ya kifo chake kwa ajili ya watu ambao wanastahili kumiliki mali na madeni hayo kwa mujibu wa sheria.
Je, hatua gani zinaweza kuchukuliwa dhidi ya msimamizi wa mirathi asiyefuata haki, usawa na uaminifu?
Usimamizi wa mirathi hufanywa kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu. Matumizi mabaya ya dhamana ya usimamizi wa mirathi ni kosa la jinai na mhusika anaweza kushitakiwa mahakamani kwa makosa ya madai au jinai. Msimamizi anaweza pia kunyang\'anywa hadhi hiyo iwapo mahakama itaridhishwa kwamba amekiuka maadili ya majukumu yake.
Je, mahakama inaweza kugawa mali za marehemu?
Wajibu wa mahakama katika mirathi ya marehemu ni kusaidia kuthibitisha msimamizi wa mirathi na kuhakikisha mirathi hiyo imegawanywa kwa haki na usawa. Mahakama haiwezi kugawanya mali za marehemu.
Wajibu wa msimamizi wa mirathi ni nini?
Wajibu wa Msimamizi wa mirathi unajumuisha mambo yafuatayo:
-Kufungua shauri la maombi ya usimamizi wa mirathi.
-Kuainisha na kutambua mali na madeni yaliyoachwa na na marehemu.
-Kulipa na kukusanya madeni yalioachwa na marehemu.
-Kugawanya mali kwa warithi kulingana na sheria husika.
-Kuwasilisha mahakamani hati inayoorodhesha mali na jinsi zilivyogawanywa katika mahakama ambapo shauri lilifunguliwa.
Je, kunapotokea haja au ulazima wa mali za marehemu kusimamiwa wakati maombi ya usimamizi wa mirathi yanaendelea mahakamani nini hufanyika ili kulinda mali za marehemu?
Wakati maombi ya kuomba usimamizi au utekelezaji wa mirathi yanaendelea mahakamani, mwombaji anaweza kuiomba mahakama impe usimamizi wa mirathi wa muda. Msimamizi aliyepewa usimamizi wa muda anakuwa na majukumu sawa na msimamizi aliyethibitishwa au kuteuliwa na mahakama ya kukusanya na kutunza mali ya marehemu, isipokuwa hawezi kugawa mali ya marehemu kwa warithi.
Lengo la kutoa usimamizi huu wa muda, ni kulinda mali za marehemu zinazoweza kuharibika au kupotea, kuwawezesha kutimiza majukumu ya haraka kama vile matunzo kwa watoto na mjane.
Nini maana ya wosia?
Wosia ni kauli inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa hiari yake kuonyesha jinsi gani angependa mali yake igawanywe baada ya kufa kwake.
Je, wosia unaweza kutumika kutoa maelekezo ya jinsi marehemu angependa kuzikwa?
Wosia ni kauli inayotolewa na muusia wakati wa uhai wake kuonyesha jinsi gani angependa mali yake igawanywe. Kwa maelezo hayo, mwili wa marehemu sio sehemu ya mali zake na hivyo wosia hauwezi kutumika kutoa maelekezo ya jinsi marehemu angependa kuzikwa. Marehemu atazikwa kwa mujibu wa mila, desturi au dini yake.
Je, wosia unaweza kubadilishwa?
Wosia unaweza kubadilishwa wakati wowote kwa kipindi ambacho muusia atakua hai.
Je, ni sababu zipi zinazoweza kubatilisha wosia?
Wosia unaweza kubatilishwa pale ambapo itathibitika kwamba muusia amepungukiwa akili kwa sababu ya wazimu, ugonjwa, ulevi na hasira.
Je, wosia unaweza kuhifadhiwa mahali gani?
Wosia unaweza kuhifadhiwa ama kutunzwa mahali popote palipo na usalama na ulinzi ili kuepuka kughushiwa mfano;
-Ofisi ya kabidhi wasii mkuu (RITA)
-Kwenye vyombo vya kutoa msaada wa kisheria
-Asasi za kidini kama kanisani au msikiti
-Katika kampuni ya uwakili
-Kwa mtu yeyote asiye mrithi katika wosia husika
-Benki
-Mahakamani, n.k.
Ni vitu gani vya muhimu vinavyozingatiwa katika kuandaa wosia wa maandishi?
Wosia wa maandishi ni lazima uzingatie yafuatayo;
-Uandikwe kwa kalamu ya wino usiofutika kwa rahisi.
-Anayetoa wosia lazima awe na akili timamu.
-Wosia utaje tarehe ulipoandikwa.
-Wosia utaje kuwa anayetoa wosia anafanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe.
-Wosia ushuhudiwe na mashahidi wawili wanaojua kusoma na kuandika. Shahidi mmoja awe wa ukoo na mwingine awe mtu baki kama muusia anajua kusoma na kuandika.
-Wosia hushuhudiwa na mashahidi wasiopungua wanne, mashahidi wawili wawe wa ukoo na wawili wawe watu baki kama muusia hajui kusoma na kuandika.
-Wanaotarajia kurithi hawaruhusiwi kushuhudia wosia huo.
-Wosia utiwe na saini ya muusia mbele ya mashahidi wake au kama hajui kusoma na kuandika aweke alama ya dole gumba la kulia.
-Wosia utiwe saini na mashahidi.
Ni vitu gani vya muhimu vinavyozingatiwa katika kuandaa wosia wa mdomo?
Wosia wa mdomo ni lazima uzingatie yafuatayo;
-Wosia ushuhudiwe na mashahidi wanne, wawili wawe wa ukoo na wawili wawe watu baki.
-Muusia awe na akili timamu.
-Kama mashahidi watakufa kabla ya muusia basi wosia huo hautakubalika.
Je, wosia unaweza kugusia mali zisizo za marehemu?
Wosia wowote ambao unarithisha mali zisizokuwa za marehemu au ambazo zilikuwa zinamilikiwa na marehemu pamoja na mtu mwingine kwa namna ya maslahi yasiyogawanyika hautakua halali.
Je, ni mazingira gani ambayo yataamua matumizi ya Sheria husika ili kushughulikia mirathi?
Yapo mazingira ya aina mbili yanayoweza kuamua ni sheria gani itumike; Kwanza, pale ambapo mtu amefariki akiwa ameacha wosia, kile kilichoandikwa katika wosia ndicho kitakachoongoza mgawanyo wa mali na madeni yake, isipikuwa kama mahakama itashawishiwa kuamini vinginevyo. Pili, pale ambapo mtu amefariki bila kuandika wosia, kwa kuzingatia aina ya maisha aliyokuwa anaishi, mirathi yake itashughulikiwa kwa namna hiyo. Kwa mfano, kama marehemu aliishi kwa utamaduni na taratibu za kiislam, Sheria ya Kiislam kuhusu Mirathi itatumika.